Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kwamba ugonjwa wa Ebola umezuka katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Msemaji wa WHO nchini humo Eugene Kabambie amesema shirika hilo limechukua hatua hiyo baada ya watu watatu kufariki wakishukiwa kuwa na Ebola eneo hilo tangu Aprili 22.
WHO imesema mlipuko huo unaathiri maeneo ya msituni ya Aketi, katika mkoa wa Bas-Uele karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Shirika hilo limesema Waziri wa Afya wa DR Congo Oly Kalenga kupitia barua, alisema kulikuwa na watu tisa kutoka eneo la kiafya la Likati, Aketi waliohofiwa kuwa na Ebola.
Watano kati yao walipimwa na mmoja wao akathibitishwa kuwa na virusi hivyo.
Watatu kati ya tisa hao walifariki.
Waziri huyo alikuwa ameiandikia WHO barua akiomba usaidizi katika kudhibiti ugonjwa huo.
"Ni kisa kilichotokea eneo lililo mbali sana, lenye msitu mkubwa, kwa hivyo tulikuwa na bahati kiasi. Huwa twachukulia kwa uzito sana visa kama hivi," alisema Kabambie.
Eneo hilo linapatikana kilomita 1,300 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa DR Congo, Kinshasa. Kitovu cha mlipuko wa sasa ni eneo la Nambwa.
Mwaka 2014, mkurupuko wa ugonjwa huo Congo ulidhibitiwa kwa haraka ingawa watu 49 walifariki.
Watu zaidi ya 11,000 walifariki kutokana na mkurupuko wa Ebola Afrika Magharibi 2014-2015, sana nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mlipuko wa Ebola ulioatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.
Mlipuko huo wa sasa ni wa nane kutokea nchini DR Congo tangu mwaka 1976.