RAISI ZUMA AWASILI TANZANIA | maendeleo media
BREAKING NEWS
Loading...

Thursday, 11 May 2017

RAISI ZUMA AWASILI TANZANIA

Image result for ZUMA IN TANZANIA TODAY
Raisi wa afrika kusni zuma



Dar es salaam , Tanzania- Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini akitua nchini jana usiku akiwa na mawaziri sita na wafanyabiashara 80, nchi hiyo imekubali kutoa mafunzo kwa marubani wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya nchi hizo mbili kuhakikisha Tanzania inakuwa na sekta ya usafirishaji iliyo imara.

Nchi hizo mbili pia zimekubaliana kuhakikisha zinarithisha kwa vizazi vijavyo historia ya ukombozi ambao nchi hizo zilishirikiana katika harakati za kujikwamua kwenye ukoloni ili isije ikapotea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema jana kuwa makubaliano ya kutoa mafunzo kwa marubani wa Tanzania ni sehemu ya mkataba wa uchukuzi ambao nchi hizo zitatiliana saini leo.

Mkataba mwingine ambao utasainiwa leo ni uhifadhi wa mazingira na uoto wa asili. Katika hotuba yake aliyoitoa kwa tume ya marais katika ngazi ya mawaziri kati ya Tanzania na Afrika Kusini, Dk Mahiga alisema mikataba hiyo ina lengo la kuzinufaisha nchi zote mbili ambazo zimekuwa na uhusiano wa kihistoria tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Nkoana Mashabane alisema kuna haja kubwa kwa nchi hizo mbili kuhakikisha historia ya ushirikiano haipotei. Alisema Tanzania imefanya makubwa kwa Afrika Kusini na ndio maana wananchi wa Afrika Kusini wanaona Tanzania ni nyumbani.

Mikataba hiyo itasainiwa leo wakati wa mkutano wa Rais John Magufuli na Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye amewasili jana kwa ziara ya kiserikali. Rais Zuma amefuatana na mawaziri sita na wafanyabiashara 80 kuonesha kuwa ziara hiyo ni ya muhimu kwa nchi hizo mbili.

“Mikataba hii inalenga nchi hizi mbili ziweze kutumia raslimali zake kwa manufaa ya watu wake,” alisema Dk Mahinga. Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi, Dk Mahiga alisema kwamba Tanzania imedhamiria kuimairisha sekta ya usafiri wa anga ndio maana imeiomba Afrika Kusini kusaidia kutoa mafunzo na hata kukarabati ndege za Shirika la Ndege la Tanzania.

Alisema Lengo la Tanzania na Afrika Kusini ni kupanua ushirikiano katika maeneo ya biashara, uchumi na uwekezaji. Dk Mahiga alisema Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi 10 ambazo zinaongoza kuwekeza nchini ikiwa inachangia katika uwekezaji wa nje kwa asilimia 10.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa kampuni 226 za Afrika Kusini zimewekeza nchini kwa thamani ya dola za marekani milioni 803.15. Alisema kampuni hizo zimeweza kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 20,916.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara wa Afrika Kusini kuja nchini na kuwekeza zaidi katika sekta mbalimbali. Dk Mahiga alisema nchi hizo mbili zimepanua ushirikiano katika maeneo ya biashara, uwekezaji, miundombinu, kilimo, elimu, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, habari, utamaduni na michezo, afya, nishati na madini pamoja na utalii na maliasili

google+

linkedin