Raisi wa Rwanda Paul Kagame alifungua kongamano hilo siku ya Jumanne na kutoa wito teknolojia kutumiwa kama mbinu ya kuliunganisha bara la Afrika katika nyanja mbalimbali.
Kongamano hili linahudhuriwa na viongozi kadhaa wa bara la Afrika pamoja na wadau wengine katika sekta hiyo.
Lengo kuu la kongamano hili ni kujadiliana namna ya kutumia teknolojia kutatua changamoto mbalimbali barani Afrika hasa kupambana na umasikini kwa lengo la kuimarisha kipato cha raia wa bara hilo kwa kuunda nafasi za kazi.
Marais kadhaa wa bara la Afrika mwaka 2013, wakiongozwa na rais Paul Kagame, Yoweri Museveni (Uganda), Uhuru Kenyatta (Kenya) miongoni mwa wengine, waliinda kamati maalum inayofahamika kama SMART AFRICA kuimarisha sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia.
Rais Kagame ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo inayotambuliwa na Umoja wa Afrika, amesema wao kama viongozi ni kutoa uongozi na kutengeza mazingira ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Ajenda kuu ya Kamati hiyo ni pamoja na:-
1. Kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika, kwa lengo la kupambana na umasikini hasa katika sekta ya elimu, afya, biashara, Kilimo miongoni mwa sekta nyingine.
2. Kuwezesha upatikanaji wa haraka wa mtandao kwa lengo la kuwafikia watu wengi na kuwezesha uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa mawasiliano kwa urahisi.
3. Kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, lengo ni kuwezesha wananchi kupata taarifa muhimu kuhusu serikali.
4. Kuweka sekta ya binafsi kwanza. Lengo ni kuwavutia wawekezaji katika sekta hii kujitokeza na kusaidia uudwaji wa nafasi za ajira lakini pia kuinua wawekezaji wa ndani.
5. Kuwahimiza wanawake na vijana kujikita katika sekta hii, ili kuinua hali zao za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha walemavu.