NECTA YAFAFANUA RUFAA ZA WALIOTUMBULIWA NA MAGUFULI | maendeleo media
BREAKING NEWS
Loading...

Thursday, 11 May 2017

NECTA YAFAFANUA RUFAA ZA WALIOTUMBULIWA NA MAGUFULI


Makundi matatu ya watumishi wa umma likiwemo kundi la watumishi walioghushi vyeti, watumishi waliowasilisha vyeti visivyokamilika na watumishi wenye vyeti vyenye utata ambavyo cheti kimoja kinatumiwa na zaidi ya mtumishi mmoja wamejitokeza kukata rufaa na kuhakiki vyeti.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeeleza kuwa umati wa wafanyakazi hao ambao tayari wameshatumbuliwa ulionekana katika ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ambapo walikwenda kukata rufaa.
Baadhi ya watumishi waliojitokeza katika eneo hilo la Necta, walioomba kutotajwa majina yao kwa usalama wao kikazi, walibainisha kuwa wameamua kukata rufaa kwa kuwa wana uhakika hawajaghushi vyeti vyao.
“Mimi nimeshangaa kuliona jina langu kwenye orodha ya walioghushi kwanza nimeshtuka sana, nimeambiwa vyeti vyangu vinatumiwa na watu wengine ambao hata siwajui, nimekuja hapa kuthibitisha kuwa mimi ndio mmiliki halali wa vyeti vyangu,” alisema mmoja wa watumishi hao aliyetambulisha kuwa anafanya kazi kwenye halmashauri.
Kwa upande wake, mtumishi mwingine aliyedai kuwa ni mwalimu, alipongeza utaratibu uliowekwa na Necta wa kusikiliza malalamiko ya watumishi na kubainisha kuwa tangu afike hapo baada ya kupewa namba amefanikiwa kuwasilisha vyeti vyake na sasa anasubiri matokeo.
Hata hivyo, mtumishi huyo alionyesha wasiwasi juu ya ajira yake na kubainisha kuwa kuwa kwa kuwa jina lake limeshaondolewa kwenye mfumo wa malipo wa mwajiri wake, huenda ikachukua muda mrefu kurejeshwa tena hivyo hali yake kimaisha kuzidi kuwa ngumu.
“Kiutaratibu sisi Necta tunatakiwa kuwashughulikia watumishi waliopo kwenye orodha ya vyeti vyenye utata, tunamtaka mtumishi aliyekata rufaa awasilishe vyeti vyake halali kwetu tunampa namba na anaondoka zake,” amesema Afisa Habari wa NECTA John Nchimbi Jumatano.
Amesema kiutaratibu watumishi ambao vyeti vyao havijakamilika, wanatakiwa kuwasilisha rufaa zao kwa waajiri wao na vielelezo kamili.
Nchimbi amesema kuwa ni juu ya waajiri kuwasilisha mbele ya baraza hilo rufaa hiyo itakayo ambatana na vielelezo hivyo kamili.
Lakini Baraza la Mitihani limesema kuwa watumishi wenye vyeti vya kughushi wanapaswa kuwasilisha rufaa zao kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala wa Bora ambaye ndiye atakayewasilisha rufaa hizo kwa baraza hilo la mitihani.
“Bahati mbaya kwa sasa wote wanakuja kwetu lakini tunawahudumia, tunajitahidi kuhakikisha kila mtu anapata haki yake, utaratibu mzijma ukikamilika kwa tarehe iliyotangazwa na Rais John Magufuli, tutapeleka idadi ya waliokata rufaa na matokeo kunakohusika,” alifafanua.

google+

linkedin