Mapema mwaka huu serikali ya Tanzania ilianza kutilia mashaka utendaji wa makampuni ya kuchimba madini nchini humo hasa baada ya kuaminika kuwa kiasi kisichojulikana cha mchanga wenye madini kinatolewa nje ya nchi bila udhibiti mzuri.
Serikali ya Rais John Pombe Magufuli iliunda tume ya uchunguzi kufuatilia suala hilo na mwezi uliopita matokea ya uchunguzi huo yalionyesha kuwa Tanzania imekoseshwa trillion za mapato kutokana na mauzo ya madini ya mchanga unaotolewa nje na makampuni hayo.
Moja ya kampuni kubwa iliyomulikwa katika mgogoro huo ilikuwa Acacia ambayo kampuni yake mama ni Barrick Gold Corporation yenye makao yake makuu nchini Canada. Barrick Gold ni moja ya kampuni kubwa sana za uchimbaji madini duniani ikiwa inaendesha uchimbaji katika mabara yote ya dunia.
Sasa imedhihirika kuwa kampuni hiyo imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya kimikataba na mwenendo mbaya wa shughuli za uzalishaji katika nchi kadha ambako kampuni hiyo ina machimbo ya madini.
Uchunguzi wa Idhaa ya Kiswahili VOA unaonyesha kuwa nchi nyingi katika mabara ya Asia, Afrika na Amerika ya Kati zimekuwa na migogoro ya kimikataba na madai ya uharibifu wa mazingira dhidi ya Barrick Gold. Pia kumekuwepo na madai ya udhalilishaji wa wafanyakazi katika machimbo yanayomilikiwa na Barrick Gold.
Kama ambavyo serikali ya Tanzania imetaka mikataba na makampuni ya madini – ikiwemo Acacia - irejewe upya na kufanyiwa marekebisho, serikali ya Jamhuri ya Dominica nayo inadai kuwa mikataba kati yake na Barrick Gold ina athari mbaya kwa taifa hilo la Caribbean.
Idara ya forodha nchini Dominica imetuhumu Barrick Gold kwa “mwendelezo wa kukiuka utaratibu wa kukamilisha kujaza fomu za kusafirisha nje madini ya dhahabu.”
Mwaka 2009 gazeti la This Day la Tanzania liliripoti madai kwamba kampuni ya Barrick Gold iliwacha kemikali zinazotumika katika uchimbaji kuchanganyika na vyanzo vya maji katika mkoa wa Mara na hivyo kutishia maisha ya wakazi wa mkoa huo.
Huko Pakistan mwaka 2012 mahakama ya juu ilibatilisha hati ya kukodisha ardhi waliyopewa Barrick na kampuni nyingine ya Madini Antofagasta ya Chile. Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, hatua hiyo ilifuatia madai kuwa eneo hilo lina dhahabu na shaba nyingi kuliko sehemu yoyote duniani. Kampuni hizo zikafungua mashauri katika kesi ya upatanishi wa kimataifa na mpaka hivi leo mgogoro huo haujatatuliwa.
Mwaka 2009 gazeti la The Star, la Toronto, Canada liliripoti kuwa wakati Barrick iliponunua Placer Dome, ilirithi mgogoro uliokuwepo muda mrefu katika eneo la uchimbaji la Porgera Valley, Mwaka 2006. Gazeti hilo lilielezea mgogoro huo kuwa kama ni “eneo la kivita, ambapo mamia ya wanakijiji walikuwa wamekabiliwa na walinzi wa mgodi zaidi ya 400 na polisi katika ugomvi uliopelekea umwagaji damu” ambao ulisababisha watu wanane kuuawa.
Mwaka 2003 taarifa iliyotolewa na taasisi ya haki za binadamu, Lake Cowal Campaign ya Sydney,Australia ilidai kuwa sumu ilivuja katika ngome ya machimbo ya Barrick huko Australia Magharibi ambayo Barrick ni mshirika.
Nchini Argentina gazeti la IPS news la Santiago liliripoti kuwa Barrick ililazimika kusitisha mpango wa kuchimba dhahabu katika Mlima Famatina kwenye jimbo la La Rioja kufuatia maandamano yaliyofanywa na jamii nzima na kashfa ya ufisadi iliyomhusisha gavana wa jimbo ambaye alikuwa anausaidia mradi huo. Polisi waliripotiwa kuwashambulia waandamanaji.
Chanzo cha habari cha La Republica nchini Peru kiliripoti uvunjifu wa sheria ulitokea Peru mwaka 2006 wakati waandamanaji wakidai mazingira bora ya kazi katika eneo la machimbo ya Barrick huko Pierina, yalipopelekea watu wawili kupoteza maisha katika mikono ya polisi.
Nchini Marekani pia tangu Barrick ilipochukua machimbo makubwa ya Goldstrike na eneo la kuchenjua madini katika jimbo la Nevada miaka 1980 kumekuwa na malalamiko kuhusu athari za operesheni zao kwa mazingara. Mwaka 2005 gazeti la New York Times lilichapisha habari ukurasa wa mbele ikitumia kigezo cha machimbo hayo jinsi yanavyo athiri kwa kiwango cha juu matatizo ya maji yanayo sambazwa na serikali wakati kampuni hiyo ikizalisha sumu zinazotokana na masalio ya mercury kuliko kiwanda chochote kingine.