Wawekezaji Tanzania washtushwa na hatua ya Magufuli | maendeleo media
BREAKING NEWS
Loading...

Thursday, 29 June 2017

Wawekezaji Tanzania washtushwa na hatua ya Magufuli





Miswada mitatu itayokayo walazimisha makampuni yanayochimba madini na nishati nchini Tanzania kurekebisha mikataba yao ni hatua ambayo imewashtua wawekezaji wa kigeni.

Miswada mitatu
Miswada mitatu iliwasilishwa na serikali ya Tanzania kwenye Bunge Alhamisi ambayo itairuhusu kuyalazimisha makampuni yanayochimba madini na nishati kufanya mazungumzo juu ya kurekebisha mikataba yao.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa haikufahamika mara moja ni jinsi gani pendekezo la mazungumzo hayo juu ya mikataba litaathiri mradi wa Dola za Marekani bilioni 30 wa gesi, au sekta ya madini iliyoko tayari mashakani, ambayo inaiingizia Tanzania pato la asilimia 3.5 la uchumi wake wa ndani.
Malalamiko ya wafanyabiashara
Wafanyabiashara wamelalamika kuwa wanahisi Rais John Magufuli anawabana pasipo na haki kupitia tafsiri kadamizi za sheria za kodi, ikiwemo ongezeko la faini na madai ambayo wamekuwa wakiyaorodhesha kwa haraka katika soko la hisa la ndani ya nchi.
Lakini Magufuli anasema mageuzi hayo yataongeza uwazi na pato la taifa na kuwa makampuni yamekuwa hayalipi kodi stahili, madai ambayo wao wanayakanusha.
Miswada hiyo inategemewa kufanyiwa kazi haraka na bunge, na itawaathiri makampuni ya kimataifa na itafuatiwa na mapendekezo ya kamati inayofanya uchunguzi wa biashara ya machimbo ya dhahabu inayoendelea katika nchi hii ya Afrika Mashariki.
Marekebisho ya Sheria
Kamati hiyo imezitaka kufanyiwa mabadiliko ya haraka sheria zinazosimamia shughuli za uchimbaji madini, gesi na kodi.
Miswada hiyo mitatu inahusisha mikataba ya rasilmali asilia, mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa maliasili na marekebisho ya sheria zilizopo na kuiwezesha serikali kufanya mazungumzo tena au kusitisha mikataba.
Makampuni ambayo yataathirika ni pamoja na BG Group, ambayo ni sehemu ya Royal Dutch Shell, Exxon Mobil, Statoil na Ophir Energy.
Kampuni hizi zilikuwa na mpango wa kujenga kituo cha kusafirisha gesi nje (LNG) kitachogharimu dola bilioni 30, ikishirikiana na Kampuni ya taifa ya Tanzania Petroleum Development Corp.
Mswada wa utajiri asilia na rasilmali unasema: “Pale ambapo serikali imetoa taarifa ya kusudio la kuzungumzia tena utaratibu au makubaliano… na upande wa pili ukashindwa kukubaliana kujadiliana upya makubaliano ya masharti yasiokubalika au makubaliano hayakuweza kufikiwa… mahusiano yaliokuwepo yatasitishwa na kuchukuliwa kwamba yamefutwa.”
Inaeleza kuwa “masharti yasiyokubalika” ni kitu chochote ambacho ni “ kinyume cha maadili mazuri na utekelezaji wake unahatarisha maslahi ya watu” wa Tanzania.
Kikao cha Bunge
Hata hivyo kikao cha bunge kinachoendelea mjini Dodoma kimeongezewa muda wa siku kadhaa ilikuruhusu watunga sheria kupitia kwa makini miswada hiyo na kuipitisha, Spika wa Bunge la Taifa Job Ndugai amesema.
Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji mwingi wa dhahabu katika Afrika na imegundua maeneo makubwa yenye gesi lakini bado imebakia kuwa moja ya nchi maskini duniani.
Makampuni ya madini ambayo yanaweza kuathirika na mabadiliko ya sheria yaliyopendekezwa ni pamoja na AngloGold Ashanti, Acacia Mining Plc na Petra Diamonds.
Acacia ambayo inashughuli zaidi za uchimbaji Tanzania imekuwa ndio inayolengwa kutokana na Magufuli kukereka nayo.
Thamani ya hisa zake zimeporomoka nusu yake tangu Machi 3, wakati serikali ilipotoa katazo la kusafirisha madini kufuatia mgogoro wa kodi.
Acacia na AngloGold zimesema kuwa wamekuwa wakiipitia miswada hiyo. Mazungumzo kati ya Acacia na serikali kuhusu katazo la kusafirisha madini nje “bado hayajaanza.”
Matatizo ya Barrick Gold Corporation nchi zinazoendelea
Baada ya Rais John Magufuli wa Tanzania kupiga marufuku kampuni ya Acacia Mining kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi mwezi Aprili, mwaka huu, wachambuzi wameanza kumulika kampuni mama ya Acacia, ambayo ni Barrick Gold Corporation, na kuibua matatizo mengine ya kimikataba na mwenendo mbaya wa kazi katika nchi kadha ambako kampuni hiyo inafanya machimbo.
Uchunguzi wa Idhaa ya Kiswahili VOA unaonyesha kuwa nchi zipatazo tano katika mabara ya Asia, Amerika Kusini na Ulaya zimekuwa na migogoro ya kimikataba na hata madai ya udhalilishaji wa wafanyakazi katika machimbo yanayomilikiwa na Barrick Gold Corporation.
Kama ilivyo kwa serikali ya Tanzania ambayo imetaka mikataba irejewe upya na kufanyiwa marekebisho, Serikali ya Jamhuri ya Dominica, inatambua kuwa mkataba kati yake na Barrick Gold Corporation ni wenye madhara kwa mustakbali wa taifa hili la Caribbean. Hivyo basi, hivi karibuni, ujumbe mzito wa Barrick Gold uliwasili nchini humo kukutana na maafisa wa serikali ya Dominica ilikufanya mazungumzo, shirika la habari la Reuters limeripoti.
Serikali ya nchi hiyo imesema kuwa ilikuwa inataka kufanya mazungumzo tena juu ya mikataba hiyo kufanya makubaliano kuwa yenye manufaa kwa nchi hiyo, lakini rais wa nchi hiyo alikiri kuwa “mazungumzo haya yanahitaji kutafuta mwafaka ambao utaziridhisha pande zote.
Mgogoro wa Barrick Gold Corporation huko Dominica
Kama ilivyokuwa kwa Tanzania, kuzuia makontena 262 yenye mchanga wa dhahabu yaliyokuwa yamehifadhiwa katika bandari kavu, nchini Tanzania, serikali ya Dominica kwa upande wake, kupitia ofisi zake za ushuru wa forodha, imeendelea kuzuilia kilo 1,264 za dhahabu, ambazo ni mali ya Barrick Gold kutosafirishwa tangu mwezi mei mwaka huu.
Kufuatia sakata hili ilikuja kubainika kuwa kampuni ya Acacia iliyokuwa inadhaniwa kuwa inamiliki migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu kwa asilimia 100 ilikuwa kinyume cha hivyo na kuwa ilikuwa haina mamlaka ya mwisho katika maamuzi ya machimbo hayo, vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeeleza.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi nchini Tanzania mara baada ya mgogoro wa usafirishaji wa mchanga wa dhahabu kuibuka, Mwenyekiti wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, Profesa John Thornton ambaye ndiye mwenye hisa kubwa akiwa mmiliki mkubwa pia wa kampuni tanzu ya Acacia Mining Limited, alisafiri kutoka Canada hadi nchini Tanzania, ili kufanya mazungumzo na Rais Magufuli. Barrick Gold Corporation ina makao yake makuu nchini Canada.
Pande zote mbili zimekubaliana kufanya mazungumzo yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili. Barrick na Serikali ya Tanzania wamekubaliana wataunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano ili kufikia makubaliano kumaliza mgogoro huu.
Tuhuma za mauaji nchini Tanzania
Lakini utafiti uliofanywa na idhaa ya Kiswahili VOA unaonyesha kuwa kampuni ya Barrick Gold Corporation imekuwa ikiangazwa kwa muda mrefu katika mabara mbalimbali duniani. Kwa mfano shughuli zao katika nchi za Africa zimekuwa zikidadisiwa na jamii mbalimbali na kutaka kuwepo uchunguzi wa kujitegemea juu ya tuhuma dhidi yake.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mining Watch, Canada uchunguzi wa kina kuhusu vifo vya raia ulifanyika. Hii ni baada ya kuwepo malalamiko mwaka 1996 kwamba dazeni ya watu ilidaiwa kuwa walizikwa hai katika mgodi wa Bulyanhulu wakati eneo hilo lilipokuwa linasafishwa ilikuwaondoa wachimbaji “haramu” kwa ajili ya kuwatengenezea njia kampuni ya Canada ya Sutton Resources, kuanza uchimbaji. Kampuni hiyo miaka michache baadae ilikuja kununuliwa na Barrick.
Mwaka 2008 Barrick ilifungua mashitaka mahakamani dhidi ya asasi isiyo ya kibiashara Quebec publisher ambayo ilichapisha kitabu kinachoitwa Noir Canada kuhusu tukio la machimbo ya Bulyanhulu. Kitabu hicho kilikuwa kinaikosoa kampuni hiyo ya uchimbaji ya Canada kwa madai ya vitendo vyake vya unyanyasaji huko Afrika. Waadishi wa kitabu hicho walidai kuwa pamoja na suala hilo kutatuliwa nje ya mahakama bado kulikuwa na ulazima kuchunguza mahusiano ya kampuni hiyo ya uchimbaji, mgogoro wa silaha na watendaji wa kisiasa barani Afrika.
Lakini katika muktadhaa huu uliofanyika nje ya mahakama Profesa wa Sheria, Montreal, Pierre Noreau na wanazuoni wengine maarufu huko Quebec na waandishi walichapisha barua ya wazi, Octoba 19, huko Le Devoir ikitahadharisha kuwa kitendo cha kulimaliza suala hili nje ya mahakama inaonyesha “kwamba tangu kesi hii kuanza ilikuwa sio hatua ya kukanusha tuhuma zilizoko dhidi ya Barrick Gold Corporation, lakini kuwafunga midomo watunzi wa kitabu na masuali yao yenye uhalali.
Lakini mwaka 2009 gazeti la This Day la Juni 30, 2009 liliripoti madai ya kuachia kwa kampuni ya Barrick Gold Corporation kemikali zinazotumika katika uchimbaji kuchafua mazingira kwa kuchanganyika na vianzo vya maji katika Mkoa wa Mara nchini Tanzania. Hili lilipelekea kutolewa wito kwa kampuni hiyo kufunga operesheni zoa. Mwaka 2010 operesheni za uchimbaji huko Bulyanhulu zilisitishwa baada ya wafanyakazi watatu kuuawa katika pango.
Silaha za moto dhidi ya raia
Aidha wanajamii walituhumu walinzi wa mgodi huo na askari polisi waliwapiga risasi watu ambao walikuwa wakitafuta dhahabu katika uchafu wa machimboni uliokuwa umemwagwa na kampuni hiyo katika jalala.
Mwandishi wa Bloomberg, Cam Simpson Mwaka 2010 walinzi wa Barrick Gold waliwaua watu wasiopungua saba ambao kampuni tanzu ya Barrick iliyokuwa inaendesha mradi huo ikielezea kuwa watu hao walikuwa ni kikundi cha “majangili waliovamia” na waliingia katika mgodi wakiwa na dhamiri ya kuiba dhahabu, na mauaji kama hayo yaliendelea kutokea siku za usoni.
Kesi zilizofunguliwa nchini Uingereza
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa pamoja na shirika la Leigh Day na Mining Watch Canada, Novemba 6, 2014, kampuni tanzu iliyokuwa inajulikana kama Acacia Mining ilikabiliwa na kesi iliyofunguliwa kwenye mahakama moja Uingereza mwaka 2014, ikituhumiwa kuhusika na mauaji hayo. Kesi hiyo hata hivyo iliamuliwa mwaka 2015 nje ya mahakama na wala haikujulikana kile kilichokubaliwa kati ya pande mbili.
Barrick Gold Corporation Zambia
Ripoti ya Bloomberg ya Oktoba 16, 2014 inasema huko nchini Zambia, mwaka huo Barrick Gold Corporation ilitahadharishwa juu ya uendeshaji wa mgodi wa uchimbaji wa shaba, walioupata kupitia kampuni ya Equinox Minerals, ilitahadharisha kuwa ilikuwa mashakani kibiashara baada ya serikali ya Zambia kuitaka kampuni hiyo kulipa mrahaba wa asilimia 20 badala ya kodi. Baada ya serikali kukubali mrahaba wa kiwango cha chini, Barrick ikaendelea na shughuli za uzalishaji.

google+

linkedin