WATU watatu akiwemo mganga wa kienyeji katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamekamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga kwa tuhuma ya mauaji ya mama mmoja.
Waliofikishwa mahakamani ni Juma Idd (25), Tatu Juma (20) wakazi wa Kijiji cha Tambalale Tarafa ya Simbo wilayani Igunga na Shida Mwanasimbila (54) ambaye ni mganga wa kienyeji mkazi wa Kijiji cha Kipungulu, Kata ya Mzibamziba, Tarafa ya Puge wilayani Nzega pia mkoani Tabora.
Akiwasomea shitaka mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Igunga, Ajali Milanzi, Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Mengo Kamangala, aliiambia mahakama kuwa Mei 25, mwaka huu saa 5 usiku katika Kijiji cha Tambalale, washitakiwa wote kwa pamoja walimuua kwa kumkata na kitu chenye ncha kali Elizabeth Charles (45) mkazi wa kijiji hicho.
Mwendesha Mashitaka aliendelea kuiambia mahakama kuwa baada ya kufanya mauaji, washitakiwa walikata kiganja cha mkono wa kulia na kuondoka nacho kusikojulikana. Alidai washitakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu 196 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Mapitio ya 2002 inayozuia kutenda makosa kama hayo.
Hata hivyo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, ambalo limeahirishwa hadi Juni 28, mwaka huu itakapotajwa tena na washitakiwa wamepelekwa gerezani.