Serikali ya Kenya inazungumza na Tanzania kufungua mipaka yake, ili kuruhusu mahindi iliyonunua nchini Zambia kufika nchini mwake.
Hatua hii imekuja baada ya Tanzania kuzuia usafirishwaji nje ya nchi mazao ya chakula kwa lengo la kulinda hifadhi yake ya chakula.
Mkurugenzi wa mazao katika Wizara ya Kilimo nchini Kenya Johnson Irungu, amesema mazungumzo hayo yanaongozwa na Wizara ya Mambo ya nje ili kufanikisha ombi hilo.
Zambia imekubali kuiuzia Kenya tani 55,000 ya mahindi lakini kuzuiwa kwa mazao kutoka nchini Tanzania, kumezua changamoto ya kufika kwa bidhaa hiyo inayohitajika sana nchini humo.
Gazeti la Kikanda la kila wiki la The East African, linaripoti kuwa ikiwa mwafaka hautafikiwa mahindi hayo huenda yakasafirishwa kupitia njia ndefu ya Rwanda na Uganda kabla ya kufika nchini Kenya.
Kenya inakabiliwa na uhaba wa unga wa mahindi na imekuwa ikinunua mahindi hiyo kutoka nchi jirani ya Tanzania na Uganda kwa muda mrefu lakini kwa mwaka huu, kutokana na nchi hizo pia kukabiliwa na upungufu wa bidhaa hiyo, katika maghala yao ya taifa, serikali ya rais Uhuru Kenyatta imelazimika kutafuta mahindi katika mataifa mengine.
Mbali na Zambia, nchi ya Malawi pia imekuwa ikiizuia Kenya mahindi.
Hivi karibuni, Kenya ilisafirisha mahindi kutoka nchini Mexico.