Bingwa mara 15 wa mataji mbalimbali duniani katika mchezo wa masumbwi Mmarekani Floyd Mayweather atapambana na Conor McGregor raia wa Ireland ambaye ni bingwa wa dunia wa UFC katika uzani wa Lightweight.
Waandalizi wa pambano hili wamesema mabondia hao wawili watapambana tarehe 26 mwezi Agosti mjini Las Vegas nchini Marekani.
Pambano hili limeelezwa kuwa lenye utajiri mkubwa katika historia ya mchezo huu katika miaka ya hivi karibuni. Mamilioni ya Dola za Marekani zinatarajiwa kukusanywa katika pambano hilo.
Mayweather mwenye umri wa miaka 40 ambaye alikuwa ametangaza kustaafu, atakwenda katika pambano hili akiwa anatafuta ushindi wa mapigano 50 bila kushindwa. Hadi sasa ameshinda mapigano yote 49 bila kupoteza pambano lolote.
Naye McGregor mwenye umri wa miaka 28 ambaye ameshinda mapigano 21 kati ya 24 aliyocheza, ataweka historia ya kipekee na kuharibu rekodi ya mpinzani wake ikiwa atamshinda katika pambano hilo