Rais wa Venezuela Nicolas Maduro aliagiza Jumatano wiki hii kupelekwa kwa askari 2,600 katika jimbo la Tachira, magharibi mwa Venezuela, baada ya uporaji na mashambulizi, wakati ambapo anaendelea kukabiliwa tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili na wimbi la maandamano ambayo yamesababisha kifo cha mtu wa 43.
"Nimeagiza kupelekwa kwa askari 2,000 na maofisa 600 wa operesheni maalum," alisema Waziri wa Ulinzi Vladimir Padrino Lopez kwenye televisheni ya serikali ya VTV, na kusema kuwa alitoa agizo hilo kwa kwa amri ya rais.
Siku moja kabla ya rais kwa mara nyingine tenakuongeza muda wa hali ya tahadhari ya kiuchumi, inayotekelezwa tangu mwezi Januari mwaka 2016, inayomruhusu kupunguza "mamlaka" ya katiba na kuchukua hatua maalum ya "kijamii, kiuchumi, kisiasa na kisheria. "
Usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano, maduka kadhaa yaliporwa na vituo viwili vya polisi kuchomwa moto katika jimbo la Tachira.
Machafuko pia yanashuhudiwa katika mikoa mingine ya nchi hiyo ya Amerika ya Kusini, ikiwa ni pamoja na mashariki mwa mji wa Caracas, San Antonio Los Altos, barabara kadhaa zimezuliwa na waandamanaji wanaojificha nyuso zao.
"Hatuwezi kusema kuwa ni maandamano. Ni vitendo vya uharibifu vinavyoendeshwa na watu wenye silaha", Jenerali Padrino Lopez ameshtumu.
"Lengo ni kutaka kuifanya Venezuela kuwa kama Syria na jimbo la Tachira kuwa kama Aleppo,"Jemerali Padrino Lopez aliongeza, uku akisema kuwa "hatuwezi kukubali nchi hii itumbukie katika machafuko."