Jeshi la Marekani liko tayari kuikabili Korea Kaskazini | maendeleo media
BREAKING NEWS
Loading...

Friday 11 August 2017

Jeshi la Marekani liko tayari kuikabili Korea Kaskazini




"Suluhu ya kijeshi sasa ipo, imepangwa na iko tayari, Korea Kaskazini wakidhubutu kuchukua hatua isiyo ya busara. Twatumai Kim Jong-un atachagua njia nyingine!" Trump ameandika kwenye Twitter.

Amesema hayo huku Korea Kaskazini ikimtuhumu kwa kukaribia kutumbukiza rasi ya Korea katika vita vya nyuklia.

Pyongyang inakamilisha kuandaa mpango wake wa kurusha makombora karibu na kisiwa cha Marekani cha Guam.

Idara ya mambo ya nje katika kisiwa hicho katika bahari ya Pasifiki imetoa mwongozo Ijumaa pamoja na ushauri kwa wakazi wa kisiwa hicho kuhusu jinsi ya kujiandaa kukiwa na tishio la makombora.

Idara hiyo imewaonya raia wake wajiepushe kutazama mwanga kutoka kwa kombora kwani unaweza "kupofusha".

"Lala sakafuni na ukinge kichwa chako. Iwapo mlipuko utakuwa umbali kiasi kutoka ulipo, inaweza kuchukua sekunde 30 au zaidi kwa wimbi la mlipuko wenyewe kukufikia."

Bw Trump ameandika hivyo kwenye Twitter baada ya kutishia mapema wiki hii kupitia Twitter kwamba "Korea Kaskazini wasidhubutu kutoa vitisho zaidi kwa Marekani. Watajibiwa kwa moto na ghadhabu ambayo ulimwengu haujawahi kushuhudia."

Aidha, Ijumaa, shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA liliituhumu Marekani kwa "jaribio la kihalifu la kusababisha mkasa wa kinyuklia katika taifa hilo la rasi ya Korea."

Shirika hilo lilisema Marekani inafanya kila juhudi kufanyia majaribio silaha zake za nyuklia katika rasi ya Korea.

Marekani ndiyo "mpanga njama ya tishio hili la nyuklia, mraibu wa vita vya nyuklia," taarifa ya KCNA imesema.

Awali, alikuwa ameitahadharisha Korea Kaskazini kwamba inafaa kuwa na "wasiwasi sana" iwapo itatenda lolote kwa Marekani.

Alisema utawala wa taifa hilo utakuwa shida kubwa "ambayo ni mataifa machache sana yaliyowahi kukumbana nayo" iwapo "hawatabadilika".

Kadhalika Bw Trump alikuwa awali ameshutumu serikali za awali za Marekani akisema zilionyesha udhaifu sana zikikabiliana na Korea Kaskazini na pia akashutumu mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini, akisema kwamba inafaa "kufanya juhudi zaidi."

Alisema: "Nawaambia, iwapo Korea Kaskazini itafanya jambo lolote hata kwa kufikiria tu kuhusu kumshambulia mtu tunayempenda au tunayewakilisha au washirika wetu au sisi wenyewe inaweza kuwa na wasiwasi sana, sana."

"Nitawaambia ni kwa nini...ni kwa sabbau mambo yatawatendekea ambayo hawajawahi kufikirtia kwamba yanaweza kutokea."

Hata hivyo, aliongeza kwamba Marekani bado iko huru kushiriki katika mashauriano.

Aliongeza: "Nawaambia hivi, Korea Kaskazini inafaa kujiweka sawa au wataona shida kubwa kiasi ambacho ni nchi chache sana zilizowahi kushuhudia."




Korea Kaskazini ilisema Jumatano kwamba inapanga kurusha makombora ya masafa wa wastani na ya masafa marefu kuelekea kisiwa cha Guam, ambapo kuna kambi ya ndege za kivita za kuangusha mabomu za Marekani.

Hata hivyo, kufikia sasa hakujakuwa na dalili zozote kwamba huenda kisiwa hicho cha Guam kikashambuliwa.

google+

linkedin